|
MKUU WA MKOA WA TANGA LUTENI (MSTAAFU) CHIKU GALLAWA AKIMKABIDHI MAKAMU WA PILI WA RAIS WA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR BALOZI SEIF ALLI IDD HUNDI YA SHILINGI MILIONI 11.2 KAMA MCHANGO WA RAMBIRAMBI KWA WANANCHI WA ZANZIBAR KUFUATIA KUZAMA KWA MELI YA MV. SPICE ISLANDERS ILIYOZAMA MIEZI MIWILI ILIYOPITA. |
Na Mashaka Mhando,Zanzibar
MKUU wa mkoa wa Tanga, luteni (mstaafu) Chiku Gallawa, amesema wananchi wa mkoa huo, waliupokea kwa masikitiko makubwa msiba wa wananchi waliokuwemo kwenye meli ya Mv Spice Islanders iliyozama miezi miwili iliyopita kwenye mkondo wa Nungwi Visiwani humo, na kwamba wameguswa hasa kutokana na ukaribu wake na visiwa hivyo.
Akizungumza juzi wakati wa kukabidhi rambirambi ya michango kwa ajili ya watu waliopeza maisha kwa Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi, Seif Alli Idd, Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa wanachi wa mkoa wa Tanga waliuopokea kwa masikitiko makubwa msiba huu mzito kutokana na mkoa huo kuwa na mahusiano ya karibu kutokana na kutenganishwa na bahari ya Hindi.
Alisema kuwa msiba huo utazidi kuwaunganisha wananchi wa mkoa huo na Visiwani humo katika kipindi chote cha raha, tabu na majonzi ya kuwakumbuka ndugu zao waliopoteza maisha kwenye jali hiyo na kwamba wataendelea kuwaombea ili mwenyezi Mungu awalale mahali pema peponi.
"Tanga na Zanzibar ni karibu sana na wanachi wa pande zote mbili
wana mahusiano ya karibu sana.wameguswa na msiba huu na wameomba tuwasilishe pole nyingi sana pamoja na rambirambi hii ya hundi ya sh 11,288,250, msiba huu utazidi kuwaunganisha katika kipindi chote cha raha na taabu, wameomba mwenyezi mungu aziweke mahali pema peponi roho za marehemu," alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Luteni Gallawa aliwataka wale waliokabidhiwa dhima ya kusafirisha abiria katika vyombo vya usafiri wawe wanajali maisha ya watumiaji wao na kwamba wakati mwingine majanga ya namna hiyo yamekuwa yakiepukika lakini kutokana na wasafiishaji kujaza watu kupita kiasi hupelekea matatizo ambayo husababisha maafa kama yaliyotokea kwenye meli hiyo.
Kwa upande wake Makamu wa rais, alishukuru mchango huo kutoka kwa majirani zao wa karibu na kwamba rambirambi hiyo ni kielelezo tosha cha Muungano uliotukuka baina ya wananchi wa visiwani na bara kwa kujaliana katika shida na raha hasa katika ajali hiyo ambayo haiwezi kusauliwa kutoka na uwingi wa vifo vya watu waliopoteza maisha.
"Ulikuwa ni msiba mkubwa katika historia ya Zanzibar, watu 203 walithibitika kufariki na 619 waliokolewa, serkali zote mbili ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar zilishirikana katika kipidi chote cha janga hili, na kuwasaidia wahanga hao," alisema Makamu huyo wa Rais.
Alisema tume imeundwa kuchunguza mkasa huu na serikali ya SMZ itatoa majibu yake hadharani kwa wananchi ili kuepusha janga kama
hilo lisitokee tena na kwamba michango yote itapokelewa na kutumiwa kwa makusudi kwa kadri itakavoamriwa na serikali.
Ujumbe wa Tanga kwenda visiwani humo uliongozwa na Mkuu huyo wa mkoa, pia walikuwemo Mwenyekiti wa CCM mkoa Bw. Mussa Shekimweri Mkuu wa wilaya ya Tanga Dkt Ibrahim Msengi, Mkuu wa wilaya ya Muheza Bw. Methew Nasei na mwakilishi wa wafanyabiashara mkoani Tanga Bw.Salim Abdallaziz kutoka kampuni ya unga wa ngano ya Pembe.