Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach

Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach
Kwa usafiri wa Dar es salaam, Morogoro, Dodoma na Arusha, safiri kwa raha na Simba Mtoto Luxury Coach

Thursday, February 2, 2012

MPIGA PICHA MAARUFU MKOANI TANGA ELIAS NGOSWE, AGONGWA AKIPIGA PICHA KWENYE MAHAFALI

Mmoja wa majeruhi waliogongwa na gari lenye namba T489 AGJ aina ya Toyota Bw. Elias Ngole almaarufu Ngoswe ambaye ni mpiga picha maarufu mkoani Tanga, aliyefika kwenye mahafali ya kidato cha sita katika shule hiyo ya Korogwe Girls akiwa amepakiwa kwenye bajaj kukimbizwa katika hospitali ya Magunga kwa matibahu.

Mwanafunzi Renata Renatus anayesoma kidato cha sita katika shule hiyo, akiwa katika hospitali ya Magunga wilayani Korogwe akihudumiwa na muuguzi alipofikishwa katika hospitali hiyo.

Gari lililosababisha ajali likiwa limebenuliwa ili kuwatoa majeruhi wa ajali hiyo ambayo imeleta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi na wazazi waliofika.

Mkuu wa wilaya ya Korogwe (mwenye suti nyeusi) akiwa amemshika mwanafunzi Kibibi Mmasa (19) ambaye ndiye aliyeendesha gari hilo kwa kuliweka gea kisha gari hilo kurudi nyuma na kuwagonga wanafunzi wenzake na kuwasababisha majeraha makubwa 

Mwanafunzi Zahra Jumanne (19) akipelekwa wodini baada ya kupatiwa matibabu mwanafunzi huyo ni mmoja ya wahitimu walioumia sana.

Mwanafunzi Nancy James akiwa amelazwa katika hospitali hiyo ya Magunga akipatiwa matibabu na wauguzi wa hospitali hiyo.
Na Mzee wa Bonde,Korogwe
VILIO, majonzi na huzuni vilitawala leo asubuhi katika shule ya sekondari ya Wasichana Korogwe, kufuatia wanafunzi wapatao saba na mpiga picha mmoja wa kujitegemea, kujeruhiwa vibaya kwa kugongwa na gari lililokuwa likichezewa na mmoja ya wahitimu wa kidato cha sita aliyeweka gia ya kurudi nyuma na kisha gari hilo, kuwagonga wahitimu hao.

Tukio hilo lililotokea majira ya saa 10:20 asubuhi katika shule hilo, baada ya mwanafunzi mmoja Kibibi Mmasa anayesoma kidato cha sita shuleni hapo, kuingia katika gari la kaka yake lenye namba za usajili T489 AGJ ambaye alifika kushuhudia mahafali hayo, aliweka gia hiyo kisha gari hilo kurudi nyuma kwa mwendo kasi wa kilomita 120 kwa saa na kuwaparamia wahitimu hao waliokuwa wamejikusanya vikundi.


Wanafunzi waliojeruhiwa na hali zao kuelezwa zipo katika hali mbaya ni Zahra Jumanne (19) na mpiga picha wa siku nyingi Bw. Elias Ngole 'Ngoswe', wengine ni Renata Renatus (25), Sophia Godfrey (19), Victoria Mtwale (19), Nancy James (19) na Mwanamkonda Kapunda (19) ambao wote wanasoma kidato cha sita na ambao walikuwa wakitarajia kufanya mahafali ya kumaliza shule.


Mwandishi wa habari hizi alishuhudia gari hilo likiendeshwa na mwanafunzi huyo likitembea kwa kasi kurudi nyuma na kuanza kumgonga mpiga picha huyo ambaye alikuwa akizungumza na Mwandishi wa ITV na Redi One Bw. William Mngazija ambaye baada ya kuliona gari hilo aliruka pembeni lakini mwenzake alishindwa na badala yake gari hilo lilimgonga kisha kunasa chini yake na kuburuzwa hadi kiasi cha mita 30 gari hilo lililopogonga mti na kusimama.


Baada ya kugongwa mpiga picha huyo liligonga wanafunzi wengine ambao walikuwa wamejikusanya wakibadilishana mawazo namna watakavyosherehekea mahafali yao ambayo mgeni rasmi alikuwa ni Mkurugenzi wa benki ya posta nchini Bw. Sabasaba Moshingi ambapo mmoja Zahra aligongwa vibaya na kunasa chini ya gari hilo ambapo gari hilo lilipinduliwa ili kumnasua huko chini akiwa amevunjika miguu na kupata jeraha kubwa kichwani.


"Kaka alinituma mle ndani ya gari wakati nikichukua mzigo aliyonituma ghafla nikaona gari linakwenda, nikawa sijui kinachoendelea nikasikia makelele wenzangu wanapiga huko nje huku nikiwa nimekanyaga mafuta," alisema Kibibi huku akisihi viongozi wamweche kaka yake ambaye alishikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo. Kaka yake ni Hussein Mmasa.


Akizungumzia tukio hilo, Bw. Mngazija alisema kama si kupata ujasiri kuwa kusogea kulipisha gari hilo pengine naye angekuwa miongoni mwa watu waliojeruhiwa lakini ana mshukuru mungu kukwepa ajali hiyo.


"Nilikuwa nasalimiana na Ngoswe hatujaonana muda mrefu, sasa ghafla nikaliona gari linakuja kwa kasi nikaruka na kumuacha mwenzangu ambaye alisogea kwa nyuma badala ya kulikwepa matokeo yake likamgonga," alisema Bw. Mngazija na kuongeza kwamba alikwepa gari hilo likiwa limemfikia hatua mbili tu na kama siyo kuitwa kuelezwa gari kuja uswa wao, lingemgonga.


Mkuu wa wilaya ambaye alifika kwenye eneo hilo na baadaye kwenda hospitali kushughulikia tiba ya wanafunzi hao, alisema tukio hilo ni la kusikitisha na alishawahi kutoa taadhali kuhusu magari yanayokwenda kwenye sherehe kama hizo shuleni kwamba magari yaegeshwe kwenye maeneo maalum kuliko kuwekwa katika maeneo kama hayo ambayo yanaweza kutokea ajali kama hizo.


Wanafunzi hao, wamelazwa katika hospitali ya Magunga wilayani hapa wakiendelea kupatiwa matibabu huku mmoja wao Zahra akiwekewa mtambo wa kumuongezea kupumua Oksijeni na wengine hali zao zinaendelea vizuri. Mahafali yaliendelea lakini hayakuwa na furaha kutokana na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment