KATIBU WA SHIRIKA HILO BI DORO EZEKEL NTUMBO AKIWA KATIKA MAHOJIANO NA MWANDISHI WA HABARI HIZI KATIKA OFISI YAO ILIYOPO KATIKA JENGO LA READ CROSS
Na mzee wa Bonde,Tanga
SHIRIKA la Unite Tanzania linalojihusisha na afya ya mtoto na sanaa, limeandaa warsha kwa watendaji na wananchi katika kata ya Usagara Jijijini Tanga yenye lengo la kuijengea uwezo jamii kuhusu masuala yanayohusu haki mbalimbali za watoto ili waweze kuzitekeleza katika familia.
Sanjari na hilo, shirika hilo litaendesha kampeni kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo mabonanza ya watoto kwa kipindi cha miezi sita lengo likiwa kuhakikisha inapambana na vitendo vinavyowakosesha raha na haki watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Bi Irene Mhando, akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, alisema kuwa lengo la mradi huo uliofadhiliwa na mtandao wa mashirika ya kiraia ya Foundation For Civil Society, alisema kwa kipindi cha miezi sita watajikita katika kata hiyo kuzungumzia kwa undani haki anazostahili kupata mtoto na vile vile kutambua vipaji vyao.
Alitaja makundi ambayo watakutana nayo katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na watendaji wa mitaa, madiwani, polisi na wananchi wa kawaida katika mitaa mbalimbali ya kata hiyo ambapo wanatarajia kwamba itawajengea uwezo wa kutambua kwa nini jamii inapaswa kuwalea watoto kwa mtizamo mpana.
"Shirika litaendesha mradi wa kampeni ya haki ya mtoto katika kata ya usagara, kwa kipindi cha miezi sita watazungumza na wananchi, watendaji, polisi na makundi mengine ya jamii ili kuhakikisha malengo ya kuijengea uwezo jamii yanatimia ipasavyo na watoto wanaishi kama watu wengine," alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, Katibu wa shirika hilo, Bi Doro Ntumbo, akijibu suala la kwanini wamechagua kata ya Usagara na siyo kata nyingine za Jiji hilo, alisema kuwa kata hiyo imekuwa na matukio mengi ya unyanyasaji wa mtoto hivyo kuendesha kampeni katika kipindi hicho kutasaidia kuongeza uelewa kwa jamii na matukio hayo mwisho wa siku kupungua.
"Ukitazama malengo ya mradi huu, kuwaongezea uelewa jamii kuhusu sera ya mtoto ya mwaka 2008, kubadilisha tabia za watu kuhusu namna wanavyotakiwa kuwapa haki watoto...Sasa kata ya Usagara tumeonelea tuanze nayo kwa vile masuala ya unyanyasaji yamekuwa yakikithiri hivyo kufika kwetu tutasaidia maana pia tutaunda mabaraza ya watoto, hii itasaidia kupunguza matukio ya ukiukwaji wa sheria za haki za mtoto," alisema Bi Ntumbo.
|
|
| | | | |
No comments:
Post a Comment