Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach

Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach
Kwa usafiri wa Dar es salaam, Morogoro, Dodoma na Arusha, safiri kwa raha na Simba Mtoto Luxury Coach

Wednesday, October 27, 2010

'Wanafunzi someni mtimize ndoto zenu'

Na mashaka Mhando,Tanga
WANAFUNZI wametakiwa kuwa makini kwa kujiwekea malengo katika muda wote wawapo shuleni ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza ndoto zake kwa kuamua akiwa shuleni anataka kuwa nani mara amalizapo masomo yake.

Sanjari na hilo pia wanafunzi wametakiwa kujiepusha na vishawishi vitakavyowafanya washindwe kusoma hivyo ili kuvishinda wanatakiwa kuwa karibu na kufungamana na dini zao ambazo zitawaepusha na ugonjwa hatari wa ukimwi.

Akizungumza kwenye mahafali ya sita ya Shule ya Sekondari Wasichana ya Mtakatifu Christina, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Sokoine Profesa Aponilea Pereka alisema kuwa kumaliza kidato cha nne siyo mwisho wa harakati zao za kusoma hivyo ni vema wakalenga kuendelea na elimu ya juu itakayowahakikishia maisha bora.

"Mimi kama mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo nina wakaribisha sana hususan kwenye kitivo cha tiba ya mifugo ili mpate shahada na kuwa madaktari wa mifugo...Lakini hamuwezi kutimiza yote hayo kama mtashindwa kujiepusha na vishawishi vitakavyowaondolea ndoto zenu," alisema Profesa Pereka.

Awali akizungumza kwenye mahafari hayo Kaimu Mkuu wa shule hiyo Bi Mariam Pendo alisema moja ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili ni tatizo la wanafunzi kuwa na simu ambazo mara nyingi wamekuwa wakiwasiliana katika muda wa kujisomea hatua ambayo inawafanya washindwe kukabiliana na masomo.

"Tatizo la wanafunzi kuwa na simu shuleni watu wanaopaswa kulaumiwa ni wazazi, kwasababu wao ndiyo wanawanunulia na kuwapa kwa ajili ya mawasiliano, lakini shule yetu inauangalizi mzuri kuwapa simu wazazi watoto ni kuwafanya washindwe kusoma badala yake wanapiga na kusikiliza simu," alisema Bi Pendo.

Aidha, Mkuu huyo wa shule alisema kuwa tatizo jingine ni suala la vitabu vya kiada katika soko ambapo vitabu vingi vilivyopo sio imara na hivyo kusababisha gharama kubwa kwa shule kutokana na kununuliwa mara kwa mara kufuatia kuchakaa mapema kabla ya mihula ya mwaka kumalizika.
MWISHO

1 comment: