Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach

Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach
Kwa usafiri wa Dar es salaam, Morogoro, Dodoma na Arusha, safiri kwa raha na Simba Mtoto Luxury Coach

Friday, August 31, 2012

Polisi wamtoa kocha Mgunda kumnusuru na kipigo cha mashabiki


Na Mzee wa Bonde
KOCHA Juma Mgunda juzi alilazimika kusindikizwa na askari polisi kutoka nje ya uwanja wa Mkwakwani kumnusuru na kipigo kutoka kwa mashabiki waliokuwa na hasira kufuatia timu ya Coastal Union kufungwa bao 2-0 na Bandari ya Mombasa katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki wa kujipima nguvu kabla ya Ligi Kuu haijaanza Septemba 15 mwaka huu.

Kocha huyo baada ya mchezo huo kumalizika mashabiki waliingia uwanjani kutaka kumtia kashkash kufuatia na kipigo hicho ambacho wamedai kocha huyo hana uwezo wa kuinoa timu hiyo iliyofanya usajili wa 'kufa mtu' msimu huu baada ya kuwachukua nyota kadhaa waliotamba na timu za kubwa hapa nchini.

Askari polisi waliokuwepo uwanjani hapo waliita gari la polisi lililoingia uwanjani ambapo askari mmoja aliyevalia kiraia alishuka na kumwambia kocha huyo aingie kwenye gari hilo la polisi lakini kocha huyo alisema hawezi kuingia katika gari hilo kwa kuwa amekuja uwanjani hapo na gari lake aina ya Toyota Cresida lenye namba T 571 AZD na askari hao walimsindikiza kuingia kwenye gari hilo na kutoka huku mashabiki wakipiga kelele hatukutaki.

Miongoni mwa waliomsindikiza kuondoka uwanjani hapo ni Mwenyekiti wa mashindano wa wa shirikisho la soka nchini TFF, Wallece Karia ambaye alilaani vikali kitendo cha mashabiki hao huku akionya kwamba kitendo walichokifanya hakikuwa cha kiungwana kwani Mgunda hakuwa na tatizo lolote katika ufundishaji.

wakati mchezo huo ukiendelea kikundi cha ushangiliaji kikiongozwa na Miraj Wandi, kiliinua bango lililokuwa limeandikwa 'Mgunda linda heshima yako ya msimu uliopita, Timu huiwezi waachie wengine', bango ambalo lilikuwa likiinuliwa upande wa Kaskazini ya uwanja huo huku wakitoa maneno 'hatukutaki Mgunda', 'Tuachie timu',.

katika mchezo wa jana ambao wageni walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo huku wenyeji wakionekana kupwaya zaidi katika sehemu ya kiungo na ushambuliaji licha ya mchezaji Suleimani kasimu 'Selembe' akionekana kufurukuta pekee yake bila kupata msaidizi hali iliyosababisha wachezaji wa kiungo wa timu ya Bandari waliokuwa wakiongozwa na David Naftari na Tony Otieno na baadaye Mohamed Banka walipata bao la utangulizi dakika 27.

Bao hilo lilifungwa kwa shuti kati umbali wa mita 35 na Naftari alioukuta mpira uliorudishwa fyongo na beki Philip Matusela wa Coastal alioyeokoa mpira uliopigwa na mshambuliaji wa Bandari Thomas Mourice na mlinda mlango Rajab Kaumbo kushindwa kudaka. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilipoanza timu zote zilifanya mabadiliko ambapo Coastal waliwatoa Joseph Mahundi, Selembe na Pius Kisambale wakaingia Sudi Mohamed, Mohamed Issa na Nsa Job wakati Bandari inayofundishwa na Rashid Sheduu akisaidiwa na Razak Siwa iliwatoa Naftari, Sharrif Mohamed, Mourice na John Macharia ikawaingiza Ali Abdalah, Evan Wandera, Banka na Hussein Puzo.

Mabadiliko hayo yaliwanufaisha wageni kwani walilisakama lango la wenyeji na hatimaye dakika 88 Wandera aliipatia timu yake bao la pili kwa kichwa kufuatia mpira wa kona iliyopigwa na Puzo kutoka mashariki ya iwanja huo na kujaa wavuni, bao ambalo lilisababisha makocha wa timu hiyo kukalia kuti kavu.

Akizungumzia tukio hilo Kocha msaidizi wa timu hiyo Habibu Kondo alikiri timu hiyo kuwa katika makundi mawili katika kipindi cha karibuni ambapo lipo linalounga mkono benchi la ufundi lakini kundi jingine likiwa halitaki kocha huyo aendelee kufundisha timu hiyo hali ambayo ameizungumzia kwamba italeta tatizo endapo haitatauliwa haraka.

"Unajua ukweli ni kwamba timu imegawanyika makundi mawili wapo wanaounga mkono kocha aendelee na majukumu yake na wengine hawataki kocha awepo, sasa hali hii ni mbaya na imeingia kwa wachezaji ni bora viongozi wakatatua tatizo hili kabla hatujaanza Ligi kuliko hali hii kuendelea inawafanya wachezaji wasijiamini michezoni na katika mazoezi," alisema Kondo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo Ahmed Hilal 'Aurora', aliwataka wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo kumpa muda kocha huyo kwani timu hiyo imebadilisha karibu wachezaji wengi walicheza katika ligi ya mwaka jana hivyo amekuwa akitafuta wachezaji wakikosi cha kwanza na kufungwa katika michezo hii ya kirafiki timu hiyo imekuwa ikitazama makosa yake.

"Wanachama lazima watulie kwanza wajue wao sio wanaomlipa kocha huyu kocha analipwa na mfadhili ambaye anakubali ufundishaji wa kochas huyu...Lakini jingine lazima wajue tumsajili wachezaji wengi hivyo kocha anawatazama wote kupata wachezaji ambao watakuwa wa kikosi cha kwanza na kufungwa ni sehemu ya kujifunza," alisema Mwenyekiti huyo huku akiwataka wanachama wafuatilie taarifa za klabu hiyo kwenye vyombo vya habari watasikia.

Coastal huo ulikuwa ni mchezo wake wa nne ambapo ilifungwa na timu hiyo ya Mombasa mabao 3-2 mjini Mombasa, kisha walisafiri na kufungwa bao 1-0 na polisi Morogoro, ikaifungwa JKT Orjoro bao 1-0 na juzi ilifungwa bao 2-0. Timu hiyo Jumamosi itacheza na Yanga kwenye uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam kabla ya Jumapili kwenda Visiwani Zanzibar ambako itakaa huko kwa wiki moja kucheza michezo ya kirafiki na timu za huko.
MWISHO

No comments:

Post a Comment