Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach

Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach
Kwa usafiri wa Dar es salaam, Morogoro, Dodoma na Arusha, safiri kwa raha na Simba Mtoto Luxury Coach

Sunday, December 12, 2010

AZAM WAFUNGA UWANJA WA MKWAKWANI KWA AJILI YA UKARABATI SEHEMU YA KUCHEZEA 'PITCH', LENGO NI KUENDELEA KUUTUMIA MZUNGUKO WA PILI WA LIGI KUU


MAFUNDI NA VIONGOZI WA AZAM FC AKIWEMO MENEJA WA UWANJA WA MKWAKWANI MBWANA MSUMARI (wa kwanza kushoto) WAKIANGALIA MAFUNDI WAKIENDELEA NA KAZI ZA UKARABATI WA PITCH YA UWANJA HUO AMBAO UMEFUNGWA TANGU NOVEMBA 26 MWAKA HUU.
Na Mzee wa Bonde,Tanga
TIMU ya Azam ya Jijini Dar es salaam, imeanza kurekebisha sehemu ya kuchezea (Pitch) ya uwanja wa Mkwakwani ili waweze kuendelea tena kuutumia uwanja huo katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza Januari 16 mwakani baada ya sehemu ya uwanja huo baadhi ya sehemu zake kuwa kipara kiasi cha wachezaji kushindwa kumiliki mpira.

Kutokana na timu hiyo ambayo imekubali kuutumia tena uwanja huo kama ilivyofanya katika mzunguko wa kwanza baada ya uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam kufungwa kupisha sherehe za kuapishwa kwa Rais, tayari umefungwa tangu Novemba 26 ambapo wataalamu wawili kutoka Dar es salaam wameanza kazi ya kuchimbua sehemu hiyo ya kuchezea ili waweze kupanda nyasi mpya.

Meneja wa uwanja huo, Mbwana Msumari aliwataja wataalamu hao kuwa ni Athumani Madenge na Idrisa Nassor ambao wanashirikiana na baadhi ya mafundi waliopo Jijini hapa kuahakikisha kwamba uwanja huo unarudi katika hali yake ya zamani ambao nyasi zake zilikuwa imara na hakukuwa na vipara.

Meneja huyo wa uwanja ambaye pia ni mwenyekiti wa Matawi ya Simba mkoani Tanga, alisema kuwa kazi inayofanyika kwa sasa ni kuchimbuliwa sehemu ya kuchezea yote na kuwekwa udongo mpya na mbolea maalumu kwa matuminzi ya uwanja na kisha kuoteshwa nyasi nyingine mpya ambazo zimetokea Mombasa nchini Kenya ambazo katika kipindi kifupi kijacho zitakuwa zimeshika vizuri tayari kwa mikimiki ya ligi hiyo na nyinginezo.

"Uwanja umechimbuliwa wote na kuwekwa udongo na umeoteshwa nyasi kutoka Mombasa, nyasi hizi zitaota kwa muda mfupi na uwanja wetu utakuwa bora kama zamani, hii ni hatua kubwa ambayo tunawashukuru sana wenzetu wa Azam kwa kuthamini na kutuunga mkono katika uwanja huu haya ni mafanikio ambayo watu wa Tanga tunatakiwa kuwaunga mkono bila kujali kwamba hii ni timu ya mkoa mwingine," alisema Msumari ambaye amekuwa mmoja ya wana michezo wenye ubunifu na mipango ambapo pia amefanikisha uwanja huo kupata kisima ambacho kitakachoondoa tatizo la ukosefu wa maji mara kwa mara.

hata hivyo, Meneja huyo aliviomba vilabu vingine visisite kuutumia uwanja huo kutokana na kuboreshwa na vile vile watu wa mkoa huo kufika kwa wingi kila inapofanyika michezo mbalimbali tofauti na maeneo mengine ambapo huwa wanafika pindi zinapocheza timu za Simba na Yanga tofauti na uwanja huo.

No comments:

Post a Comment