Na Mzee wa Bonde,Mkinga
MKUU wa mkoa wa Tanga, Meja Jenerali (Mstaafu) Said Kalembo, amesema ataingia mtaani akishirikiana na Kamanda wa polisi mkoani hapa, ACP Liberatus Sabas, kuwasaka na kuwakamata raia watatu wa kigeni, wanaorandaranda mkoani hapa bila shughuli maalum na Idara ya Uhamiaji mkoani hapa kushindwa kufanya hivyo kwa kile alichodai 'kupewa kitu kidogo'.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa iliyofanya kikao chake wilayani hapa jana, Mkuu huyo wa mkoa alisema analazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kuchoshwa na watumishi wa Uhamiaji mkoani hapa ambao amekuwa akipokea malalamiko mengi kwamba wanawaachia wageni waishi bila vibali na hata waliokuwa na vibali vilivyokwisha muda wake.
Alisema anazo taarifa kwamba wapo 'wazungu' watatu ambao wamekuwa wakizurura hovyo katika mitaa ya Jiji la Tanga, kuchukua wanawake na kuzunguka kwa visingio kuwa ni wawekezaji na wanachokifanya mkoa huo haujui lakini idara ya uhamiaji wanaohusika na uchunguzi na kuwakamata watu wa namna hiyo hawafanyi chochote badala yake wazungu hao wanatanua mitaani.
Jamani hivi hawa uhamiaji vipi, kuna siku nitaaingia mitaani kuwakamata nitamuuomba RPC huyu niwe naye nitawakamata na kuwaweka ndani, Uhamiaji wapo lakini kila mtu anasema Msuya (Danny Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Tanga) anakula rushwa...Sasa ukiona RC anaingia mtaa wakati wanaohusika wapo wanalipwa mshahara na serikali basi kuna tatizo na haiwezekani, hebu watu wa uhamiaji kama wapo shughulikieno hili ni aibu hizo rushwa zitawatokea puani," alisema Bw. Kalembo bila kuwataja wazungu hao.
Akizungumiza tuhuma hizo Bw. Msuya ambaye hakuhudhuria kikao hicho cha kamati ya usalama mkoa, alikiri kuwepo kwa wazungu hao lakini hata hivyo alikanusha kuhusika na rushwa akidai kwamba kama amekuwa akipokea rushwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ingekuwa imemkamata muda mrefu tangu malalamiko ya kupokea rushwa yanayomuandama mkoani hapa.
Aliwataja wazungu hao na kuanisha muda wa kwisha vibali vyao kuwa ni pamoja na Bw. Luitren Zijistra raia wa Uholazi anayefanya shughuli kiwanda cha maziwa na kibali chake kinamalizika Aprili 24 2012 na hana matatizo, mwingine aliyemtaja ni Bw. Zingaro Giussepe raia wa Italy ambaye kibali chake kimekwisha na Bw. Stephen Peter raia wa Ujerumani ambaye ana kibali cha Maendeleo ya Miundombinu ya Utalii.
"Unajua hawa wazungu wana vibali na huyu Stephen anakibali cha Toursim Infastructure Development amepewa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na kinaisha Februari 26 mwakani sasa anavyozunguka hapa mjini maeneo ya Mkinga huko anaonekana hana kibali kumbe la na huyu Bw. Giussepe kweli kibali chake kimekwisha na mimi nimemwandikia barua Desemba 2 kumweleza kwamba hatutamuongeza tena na huyu Bw. Luitren sioni matatizo yake, lakini kama Mkuu wa mkoa anasema labda hawakumpa taarifa vizuri," alisema Bw. Msuya.
Bw. Msuya alikiri kwamba alishawahi kuitwa na Mkuu wa mkoa ofisini kwake akaelezwa kwamba amekuwa akijihusisha na rushwa mara kwa mara madai ambayo aliyakanusha ingawa Mwandishi wa Habari hizi aliwahi kuwanukuu baadhi ya wafanyakazi wake katika ofisi hiyo ambao walidai kuwa kazi zote zinazowahusu watu weupe mkuu huyo amekuwa akizifanya yeye.
"Bosi wetu akija Mhindi utakuta anawaita ofisini kwake hataki kutuachia kwa kweli amekuwa akipenda sana kufanya kazi za watu weupe wazungu huwa anawafuata huko huko kwenye viwanda hata kama vibali vyao vimekwisha Mkuu wa mkoa hasemi uongo bosi wetu hatusemi moja kwa moja anakula rushwa lakini hata sisi anatutia mashaka," alisema ofisa mmoja wa Uhamiaji aliyekuwepo ofisini jana.
No comments:
Post a Comment