MMOJA WA MAOFISA UGANI WA KOROGWE AKIKAGUA PIKIPIKI |
MKUU WA WILAYA YA KOROGWE BW. ERASTO SIMA AKIWASHA MOJA YA PIKIPIKI HIZO HUKU MAOFISA UGANI NA WATUMISHI WENGINE WA HALMASHAURI HIYO WAKIMUANGALIA. |
MKUU WA WILAYA YA KOROGWE BW. ERASTO SIMA AKIWASHA MOJA YA PIKIPIKI HIZO. |
HARAKATI KUELEKEA MAPINDUZI YA KIJANI………
DADPS YAMWAGA PIKIPIKI KWA MAAFISA UGANI KOROGWE
Na mdau Fatna Mfalingundi,Korogwe
Katika jitihada za kutekeleza dhana ya kilimo kwanza kwa vitendo,Halmashauri ya wilaya ya Korogwe Kupitia mpango wa Maendeleo ya Kilimo wa Wilaya (DADPS) imegawa pikipiki zenye thamani ya shilingi milioni 30 kwa Maafisa Ugani sita wa Kata za Dindira, Mazinde,Vugiri,Mkalamo na katika skimu ya umwagiliaji ya Mombo.
Akitoa taarifa ya pikipiki hizo katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Mkuu wa Idara ya Kilimo,Mifugo na Ushirika Bw.Mjema Mweta alisema kuwa pikipiki hizo ni mwendelezo wa manunuzi ya pikipiki 14 ambazo tayari zimekwishanunuliwa na kwamba wanatarajia kununua sita nyingine katika mwaka huu wa fedha wa 2010/2011.
Bw.Mjema aliongeza kuwa lengo la Halmashauri ni kuwapatia Wagani wengi zaidi vyombo vya usafiri ili kuboresha ufanisi katika utendaji kazi wao ikiwemo kuwahudumia Wakulima wengi na kwa urahisi zaidi hivyo kuleta Mapinduzi ya kijani na hatimaye kupunguza umasikini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Bw.Erasto Sima aliyekuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo aliwataka Wagani hao kuzitumia pikipiki hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kuleta tija katika Sekta ya kilimo na kuonya kuwa atakayekiuka malengo na kugeuza matumizi kama vile kuzifanya “bodaboda” au nyenzo ya kuzifikia “nyumba ndogo” zake atakiona cha Mtemakuni.
Nao Wagani hao walishukuru kwa kupatiwa vitendea kazi hivyo na kueleza kuwa vitawarahisishia sana utendaji kazi na kuongeza ufanisi kwani kabla ya kupatiwa nyenzo hizo za usafiri ilikuwa ngumu sana kwao kuwafikia Wakulima wote wenye mashamba binafsi na mashamba darasa.Aidha waliahidi kuzitumia katika malengo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment