Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach

Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach
Kwa usafiri wa Dar es salaam, Morogoro, Dodoma na Arusha, safiri kwa raha na Simba Mtoto Luxury Coach

Wednesday, December 1, 2010

DKT MWAKYEMBE AFURAHI KUFANYA KAZI NA MAGUFULI, ASEMA NI MCHAPAKAZI ASIYEKUBALI KUYUMBISHWA

NAIBU WAZIRI WA UJENZI DKT. HARRISON MWAKYEMBE

     


DKT HARRISON MWAKYEMBE AKIPONGEZWA NA WABUNGE WENZAKE MARA BAADA UA KUSOMA RIPOTI YA KAMATI ILIYOUNDWA KWA AJILI YA KUCHUNGUMZA SUALA LA RICHMOND

                       Na Mdau Thobias Mwanakatwe,Mbeya
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk.Harrison Mwakyembe, amesema amefurahisha  sana na uteuzi uliofanywa na Rais  Jakaya Kikwete na hasa kutokana na kumpangia wizara moja na Mhe.John Magufuri ambaye inafahamika kuwa ni kiongozi makini na mwenye misimamo asiyekubali kuyumbishwa katika utekelezaji wa kazi za umma.
 
Amesema hayo katika mahojiano na mdau huyu kwa simu muda mfupi baada ya kuapishwa jana/juzi na Rais Jakaya Kikwete katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.
Dk.Mwakyembe alisema anajisikia vizuri sana kufanya kazi na Magufuri katika Wizara ya Ujenzi itakayoshughulikia ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege kwani ni kiongozi makini ambaye ana misimamo sana hasa katika suala la utekelezaji wa kazi za miradi maendeleo.
 
“Najisikia vizuri sana tena mno kufanya kazi na Magufuri kwani ni mtu ambaye ni mchapa kazi ambaye pia tumeshibana sana ,pia ni kiongozi ambaye ana msimamo katika kutumikia umma ambao unaeleweka asiyependa kuyumbishwa,”alisema Dk.Mwakyembe.
 
Dk.Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya, alisema kimsingi ameupokea uteuzi wa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kama changamoto kwake kwani kiongozi yeyote makini anapopewa jukumu kubwa kama la uwaziri inakuwa ni changamoto ambayo anatakiwa kuhakikisha anatimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika kuwaletea maendeleo wananchi.
 
Kuhusu ufisadi,Naibu Waziri huyo alisema kimsingi kwa kuwa suala la kupiga vita ufisadi na rushwa ni suala ambalo limetungiwa sheria kwa maana hiyo ndani ya serikali litaendelea kupigiwa kelele ili kuwepo na matumizi sahihi ya fedha za umma.
 
Dk Mwakyembe alianza kupata umaarufu kutokana na kuwa Mwenyekiti wa Kamati  Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa upatikanaji wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura, iliyopewa Kampuni ya Richmond Development LLC, ya Hauston Marekani, ambapo aliyekuwa  Waziri Mkuu, Edward Lowassa,alitajwa kuhusika kuibeba kampuni hiyo kupata zabuni.
 
Dk. Mwakyembe katika ripoti yake, aliliambia Bunge kuwa, ushiriki wa karibu wa Lowassa katika kila hatua ya zabuni ya umeme wa dharura, si lazima uwe ushahidi kwamba kiongozi huyo wa kitaifa alihusika katika kuibeba Richmond, lakini unaweza ukawa ushahidi wa staili yake ya kawaida kabisa ya uongozi katika kufuatilia masuala yote ya kitaifa kwa karibu, ikizingatiwa kwamba taifa lilikuwa katika kipindi kigumu cha ukosefu wa umeme.
 
“Mheshimiwa Spika, ushiriki huu wa karibu wa Waziri Mkuu katika kila hatua ya zabuni ya umeme wa dharura, si lazima uwe ushahidi wa kwamba kiongozi huyo wa kitaifa alihusika katika kuibeba Richmond. Unaweza pia ukawa ushahidi wa staili yake ya kawaida kabisa ya uongozi katika kufuatilia masuala yote ya kitaifa kwa karibu sana, tukizingatia kwamba nchi wakati huo ilikuwa katika kipindi kigumu sana cha ukosefu wa umeme,” alisema Mwakyembe katika hatua moja ya awali ya ripoti yake.
 
Baadhi ya hoja zilizotajwa na Dk. Mwakyembe kuwa ziliishawishi kamati yake kuamini kuwa Lowassa alihusika kuibeba Richmond kupata zabuni hiyo, ni barua ya Katibu wa Lowassa ya Juni 21, 2006, B. Olekuyan, ya kuitaarifu Wizara ya Nishati na Madini kuwa Waziri Mkuu Lowassa amekubali mapendekezo na ushauri wa Waziri wa Nishati na Madini kama ulivyokuwa umeletwa.
 
“Aidha, baadhi ya nyaraka ambazo Kamati Teule ilipata katika uchunguzi wake zilionesha kuwa maelekezo na maamuzi mengi ya msingi yalikuwa yanafanywa na Waziri Mkuu badala ya wizara. Mfano ni barua kutoka Wizara ya Nishati na Madini kwenda kwa Waziri Mkuu tuliyoinukuu ukurasa wa 31 wa taarifa hii, ikitamka wazi kuwa GNT ilifanya majadiliano na Richmond Development Company LLC tarehe 8 hadi 16 Juni 2006 “kwa kuzingatia maelekezo” ya Waziri Mkuu,” alieleza Mwakyembe.
 
Kwamba, baada tu ya kupokea barua hiyo, Waziri wa Nishati na Madini aliandika dokezo kwa Katibu Mkuu wake akimtaka aiagize TANESCO iingie mkataba mara moja na Richmond Development Company LLC baada ya Waziri Mkuu kuidhinisha mapendekezo ya wizara.
 
Dk. Mwakyembe alisema kamati yake ilibaini kuwa hisia walizokuwa nazo viongozi wa ngazi mbalimbali wa TANESCO, uongozi wa kiimla wa wizara ulikuwa ukipata nguvu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
 
Kwamba kilichoonekana ni ukiukwaji wa sheria na utaratibu mzima wa uwajibikaji, na kwamba pamoja na dharura iliyokuwa ikilikabili taifa, serikali haipaswi kuwa kinara wa kuvunja sheria za nchi.
 
Aidha, Dk. Mwakyembe alisema kuwa baadhi ya mashahidi, wakiwemo waandishi wa habari waliinyoshea kidole Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa msingi wa ubabe uliokithiri wa Wizara ya Nishati na Madini katika kuibeba Richmond.
 
Alizitaja pia baadhi ya nyaraka ambazo kamati yake ilizipata katika uchunguzi wake, zilionyesha kuwa maelekezo na maamuzi mengi ya msingi yalikuwa yakifanywa na Lowassa badala ya wizara.
 
Alitoa mfano wa barua kutoka Wizara ya Nishati na Madini kwenda kwa Waziri Mkuu iliyonukuliwa ukurasa wa 31 wa ripoti ya kamati ikitamka kuwa Juni 8, 2006 GNT ilifanya majadiliano na Kampuni ya Richmond kwa kuzingatia maelekezo ya Lowassa.
 
Dk. Mwakyembe alilieza Bunge kuwa kamati yake pia ilibaini kuwa Julai 13, 2006 Waziri wa Nishati na Madini alimwandikia Katibu Mkuu wake kumweleza kuwa kwa mara nyingine amezungumza na Lowassa juu ya bei ya mitambo ya Aggreko.
 
Katika mazungumzo hayo, Lowassa alibaki na msimamo ule ule ulioelezwa na waziri kuwa aliagiza Richmond iulizwe kama inaweza kuzalisha Megawati 40 za umeme kwa bei isiyozidi senti 4.99 za Marekani na kama ikipatikana, basi ichukuliwe Richmond.
 
Dk. Mwakyembe ambaye wakati wote wa kusoma ripoti hiyo alionekana kutamka maneno bila kumung’unya, alisema kamati yake ililazimika kuwaita kwa mara ya pili Dk. Ibrahim Msabaha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu wake, Mwakapugi, kwa ajili ya kuwahoji.
 
                                

No comments:

Post a Comment