Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach

Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach
Kwa usafiri wa Dar es salaam, Morogoro, Dodoma na Arusha, safiri kwa raha na Simba Mtoto Luxury Coach

Saturday, December 4, 2010

POLISI MBEYA WAMKAMATA MWENYEKITI WA WAFANYABIASHA KISA AMEWAZUSHIA KUIBA BIDHAA ZAO WAKATI MOTO UKIWAKA

WAFANYABIASHARA WAKIHAHA KUKIMBIZA MALI ZAO BAADA YA SOKO LA UHINDINI KUUNGUA MOTO

          NA MDAU MWANAKATWE,MBEYA 
SAKATA la Polisi kudaiwa kuiba mali za wafanyabiashara wakati soko la Uhindini, Jijini Mbeya lilipokuwa likiteketea kwa moto limeingia katika sura mpya baada ya Mwenyekiti wa soko hilo,Emily Mwaituka kukamatwa na Polisi na kufunguliwa jalada la kesi akituhumiwa kulidhalilisha Jeshi hilo.
Mwenyekiti huyo ametiwa mbaroni siku moja tu baada ya soko hilo kuungua huku wafanyabiashara wakiendelea kuomboleza kufuatia hasara ya mamilioni ya fedha waliyoipata kutokana na moto kuteketeza soko hilo juzi.
Kukamatwa kwa Mwaituka kumefuatia madai aliyoyatoa juzi na kunukuliwa na vyombo vya habari kuwa Polisi walishiriki kuiba mali za wafanyabiashara, ambazo zilikuwa zikiokolewa kutoka kwenye maduka ambayo yalikuwa hayajashika moto.
Akizungumza na blog hii muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana, Mwaituka alisema alikamatwa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, ikiwa ni muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile ili kufanya tathimini ya tukio hilo la moto.
Mwaituka alisema wakati wa kikao hicho ambacho yeye alialikwa, alisema kuwa alishuhudia kwa macho yake magari ya Polisi yakisomba mali za wafanyabiashara zilizokuwa zikiokolewa kutoka kwenye maduka ambayo yalikuwa hayajashika moto.
Alisema baada ya kumalizika kwa kikao, Kamanda Nyombi alimkamata na kumpeleka Kituo cha Polisi kati, ambako alimkabidhi kwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ili achukue maelezo yake.
Kwa mujibu wa Mwaituka, alipofikishwa kituoni hapo alitakiwa kutoa maelezo kuhusu madai aliyoyatoa, kuwa Polisi walishiriki kuiba mali za baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka yaliyopo katika soko hilo lilipokuwa linateketea kwa moto.
"Kwenye kikao mimi nilisema kuwa niliona Defender nyeupe ya Polisi ikipakia bidhaa zetu, baada ya kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kumalizika, RPC alinichukua, tukaenda naye hadi kituo cha Polisi akanikabidhi kwa Afisa wa upelelezi ili nitoe maelezo yangu, hapo nikafunguliwa jalada kuwa kwa kauli yangu ndani ya kikao eti nimelidhalilisha Jeshi la Polisi," alisema Mwaituka.
Hata hivyo Mwaituka hakutaka kuzungumzia zaidi suala hilo kwa madai kuwa ametakiwa arudi Polisi mchana kwa maelezo zaidi, ambapo aliwataka waandishi wasubiri hadi atakapototoka Polisi muda huo wa mchana.
"Tayari Polisi nimeshaandika maelezo yangu, wamesema wanaendelea na uchunguzi, hivyo wameniambia leo (jana) mchana niende tena Polisi, nawaomba msubiri nitoke huko mchana tutazungumza zaidi maana kwa sasa ninamambo mengi ya kufanya," alisema Mwaituka.
Blog hii ilipofika ofisini kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa kwa nia ya kutaka kuonana naye, alijibiwa na wasaidizi wake kuwa Kamanda Nyombi alikuwa amekwenda Tukuyu wilayani Rungwe ambako shughuli ya uchaguzi wa majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ilikuwa ikifanyika.
Hata hivyo mwandishi wa habari hii alijaribu kumpigia simu kupitia simu yake ya kiganjani, ambayo nayo ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Kufuatia kukamatwa kwa Mwenyekiti huyo wa soko, wafanyabiasha wa soko hilo wamekuja juu na kuonya kuwa kama polisi wanataka kuwasha moto wa vurugu waendelee kumsumbua mwenyekiti wao kwasababu wanaamini kuwa alichokisema kuhusu polisi kuiba mali zao ni sahihi.
Wafanyabiashara hao walisema kama Polisi wanaona wanazushiwa suala hilo serikali ya mkoa wa Mbeya iunde tume huru kuchunguza suala hilo na wao wapo tayari kutoa ushahidi.
Usiku wa kuamkia juzi, soko kuu la Uhindini, lililopo katikati ya Jiji la Mbeya liliteketea kwa moto na kuwasababishia hasara kubwa wafanyabiashara wa soko hilo.
Wakati wa tukio hilo la moto, magari mawili ya Polisi yalitumika kubeba bidhaa zilizokuwa zikiokolewa kutoka ndani ya maduka ya wafanyabiashara na asubuhi yake wafanyabiashara walipokwenda Polisi kufuatilia bidhaa zao, hawakuridhika nazo kwa madai kuwa hazilingani na zile zilizokuwa zikipakiwa kwenye magari ya Polisi.
Hivi karibuni Mwaituka alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa alipofika Polisi juzi asubuhi alionyeshwa mabegi machache, vitenge na khanga, wakati usiku hule vilikuwa vikibebwa na vitu vingine vya thamani kama vile Televisheni, Komputa, pikipiki, majenereta na vingine vingi.

No comments:

Post a Comment