WANANCHI WA JIJI LA MBEYA WAKIANGALIA MOTO UKITEKETEZA SOKO KUU LA UHINDINI LIKIUNGUA MOTO JUIZ USIKU |
BAADHI YA WAFANYABIASHARA WAKIHAHA KUTAFUTA NJIA YA KUSALIMISHA MALI ZAO KATIKA MADUKA YALIYOKUWA JIRANI NA SOKO HILO (PICHA ZOTE NA MDAU WETU EMMANUEL LENGWA) |
Na Thobias Mwanakatwe, Mbeya
SOKO kuu la Uhindini lililopo katikati ya Jiji la Mbeya limeteketea kwa moto, huku Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi wakidaiwa kushiriki kupora mali za wafanyabiashara ambao maduka yao yalikuwa yakiteketea. Hii ni mara ya pili kwa masoko makubwa kuteketea kwa moto jijini Mbeya ndani ya kipindi cha miaka minne, ambapo Desemba mwaka 2006, soko la Mwanjelwa nalo liliteketea kwa moto na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh. Milioni 800 kwa wafanyabiashara.
SOKO kuu la Uhindini lililopo katikati ya Jiji la Mbeya limeteketea kwa moto, huku Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi wakidaiwa kushiriki kupora mali za wafanyabiashara ambao maduka yao yalikuwa yakiteketea. Hii ni mara ya pili kwa masoko makubwa kuteketea kwa moto jijini Mbeya ndani ya kipindi cha miaka minne, ambapo Desemba mwaka 2006, soko la Mwanjelwa nalo liliteketea kwa moto na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh. Milioni 800 kwa wafanyabiashara.
Moto huo wa jana uliowasababishia hasara kubwa wafanyabiashara wa soko hilo ulianza juzi majira ya saa 2:20 usiku na kuendelea kuteketeza maduka huku, Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Mbeya kikishindwa kuudhibiti moto huo.
Mdau wetu aliyefika mapema kwenye eneo la tukio alishuhudia baadhi ya wamiliki wa maduka wakihaha kuokoa mali zao ambapo vibaka nao walitumia fursa hiyo kukwapua bidhaa mbalimbali za maduka ya wafanyabiashara kwa kuyavunja hasa kutokana na kutokuwepo ulinzi madhubuti.
Wakati moto huo ukizidi kutanda katika soko hilo,gari la kwanza la Kikosi cha Zimamoto lenye namba za usajili SM 6039 liliwasili eneo la tukio majira ya saa 2:40 ambapo lilijaribu kuzima moto huo kwa dakika tano tu kabla ya kuishiwa maji.
Ubovu wa miundombinu hasa njia zan kuingia ndani ya soko hilo ilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa magari ya zimamoto kufanya kazi yake, hali iliyolazimu kuleta Tingatinga ambalo lilitumika kubomoa baadhi ya maduka ili kupata njia ya magari ya zimamoto kuingia ndani ya soko na kuendelea na kazi ya kuzima moto katika maduka yaliyokuwa yakiteketea kwa moto.
Gari jingine la kikosi hicho lenye namba SM 4524 liliwasili eneo la tukio saa 2:50 ambalo nalo kama ilivyokuwa kwa gari la awali pia liliishiwa maji hali iliyozua malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walianza kuwazomea askari wa kikosi hicho kwa uzembe.
Baadaye polisi wakiwa katika gari namba T 710 APB walifika eneo la tukio na kuanza kuwakamata vibaka ambao walikuwa wamechachama kuvunja maduka na kupora mali .
Hata hivyo Polisi hao walionekana wakizunguka baadhi ya maduka kuwazuia vibaka wasiibe lakini walizidiwa nguvu kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya vibaka ambao walifika eneo la tukio wakiwa zana za kubomolea milango.
Vibaka hao walifanikiwa kubomoa baadhi ya maduka yanayouza simu za mkononi na kuzikusanya kwa kuziweka kwenye mashuka waliyokuja nayo eneo la tukio.
Katika hali ya kushangaza magari ya polisi yenye namba za usajiri PT 1464 na PT 0796 yalionekana mara kadhaa yakisomba bidhaa za maduka yaliyokuwa yamevunjwa kabla ya kufikiwa na moto huo na kuzipeleka mahali kusipojulikana huku wananchi wakiamini kuwa bidhaa hizo zilikuwa zikipelekwa kituo cha polisi.
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na mdau wa globu hii jana asubuhi, wamedai kuwa mizigo iliyokuwa ikisombwa na magari hayo ya Polisi imeyeyuka.
“Usiku ule wakati bidhaa zetu ilikuwa ikipakiwa kwenye magari ya Polisi tulijua wanatusaidia kuokoa, lakini leo (jana) tulipowafuata watukabidhi bidhaa zetu, wanatuonyesha mabegi machache tu, kwa kifupi Polisi nao wameshiriki kuiba mali zetu,” alisema Mwenyekiti wa soko hilo, Emily Mwaituka.
Mwenyekiti huyo wa soko, alisema baada ya kuona hali hiyo, waliamua kuchukua hatua za kwenda kuonana na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evance Balama ambaye aliwashauri kuwa wakamwone Mkurugenzi wa Jiji, Juma Rashid Idd kwa kuwa soko hilo lipo chini ya Halmashauri ya Jiji hilo.
Mwaituka alisema walipofika kwa Mkurugenzi wa Jiji, aliwaeleza kuwa kulikuwepo na kikao cha Kamati ya Ulinzi ya Mkoa kuhusiana na suala hilo, ambacho kilikuwa kimeitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,John Mwakipesile ofisini kwake kujadili suala hilo.
Hata hivyo mbali na magari ya Polisi, magari mengine yenye namba za kiraia nayo yalionekana katika shughuli za uokoaji wa mali, yakipakia bidhaa na kuondoka nazo.
Miongoni mwa magari yaliyoonekana yakipakia bidhaa kwenye maduka mbalimbali ni T 543 aina ya Nissan Patrol, T432 AEF, T 256 AEM, T 822, AGX, T 643 AMS aina ya Center, T 373 BBB aina ya Center, T257, ACK na T 695 ATS.
Tukio hilo la moto, lilisababisha baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa ni vibaka kutaka kujaribu kuingia katika Benki ya NMB tawi la Mbalizi Road iliyopo hatua tano kutoka sokoni hapo, hali iliyowalazimu Polisi kutumia nguvu ya ziada, ikiwemo mabomu ya machozi kuwatawanya vijana waliokuwa wameanza kujazana kwenye milango ya benki hiyo.
Tukio hilo la moto, lilisababisha baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa ni vibaka kutaka kujaribu kuingia katika Benki ya NMB tawi la Mbalizi Road iliyopo hatua tano kutoka sokoni hapo, hali iliyowalazimu Polisi kutumia nguvu ya ziada, ikiwemo mabomu ya machozi kuwatawanya vijana waliokuwa wameanza kujazana kwenye milango ya benki hiyo.
Na katika hatua nyingine, tukio hilo la moto lilimlazimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile jana kuitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi ya Mkoa kwa ajili ya kujadili suala hilo.
Baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo ya ulinzi na Usalama, Mkuu huyo wa mkoa alizungumza na waandishi wa habari na katika hali isiyo ya kawaida, alisema kuwa anawasifu Polisi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kudhibiti usalama wakati wa tukio la moto uliounguza soko la Uhindini.
“Nawapongeza Polisi kwa kazi kubwa waliyoifanya, kama sio wao hata maduka ambayo hayakuungua moto nayo yangevunjwa na vibaka, lakini pia nawapongeza Zimamoto kwa kufanikiwa kuudhibiti moto huo na mwisho naipongeza Halmashauri ya Jiji kwa ushirikiano waliouonyesha,” alisema Mwakipesile.
Alipotakiwa kuzungumzia madai ya Polisi na magari ya Polisi kushiriki kupora mali za wafanyabiashara wakati wa tukio hilo, Mwakipesile alisema mtu aliye na ushahidi autoe ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Alisema baada ya soko hilo kuteketea, ameagiza Halmashauri ya Jiji, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya na Wafanyabiashara waliothiriwa na moto huo kukaa pamoja na kuwapatia eneo jingine la kufanyia biashara wakati mipango ya kujenga upya soko hilo ikifanyika.
Alisema katika eneo hilo sasa litajengwa soko la kisasa kama ilivyo kwa Soko la Mwanjelwa ambalo baada ya kuungua hivi sasa linajengwa soko kubwa la kisasa kwa thamani ya Shilingi Bilioni 13 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya CRDB.
Mwakipesile alisema kutokana na mipango ya kujenga upya soko hilo, hata wafanyabiashara wa maduka ambayo hayakuungua moto jana nao watahamishwa ili kupisha ujenzi wa soko la kisasa katika eneo hilo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na kuwa hivi sasa timu ya wataalamu imeanza uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.
Hata hivyo taarifa za awali ambazo mwandishi wa habari hizi amezipata zinadai kuwa chanzo cha moto huo huwenda kikawa ni mamantilie wanaopika vyakula katikati ya soko hilo walisahau kuzima moto au ni hitlafu ya umeme hasa kwa kuzingatia kuwa moto huo ulianza sokoni hapo ikiwa ni muda mfupi baada ya kukatika kwa umeme katika mji wote wa Mbeya.
Jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alikataa kata kata kwa madai kuwa atatoa taarifa zaidi baadaye.
Katika hatua nyingine Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi,alifika eneo la tukio jana asubuhi kuwapa pole wahanga ambapo aliwaahidi kuwa atashirikiana nao kwa hali na mali katika kipindi hiki kigumu kuhakikisha kuwa wanapata maeneo mengine ya kufanyia biashara zao.
No comments:
Post a Comment