Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach

Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach
Kwa usafiri wa Dar es salaam, Morogoro, Dodoma na Arusha, safiri kwa raha na Simba Mtoto Luxury Coach

Wednesday, December 8, 2010

FEDHA ZA KUNUNULIA SAMANI OFISI YA MBUNGE 'WA MBEYA ZATAFUNWA' NA WAJANJA, NI OFISI YA SUGU

                         Na  Thobias Mwanakatwe,Mbeya
FEDHA zilizotengwa na halmashauri ya Jiji la Mbeya mwaka 2004/2005 kwa ajili ya  kuhudumia ofisi ya Mbunge wa Mbeya Mjini ikiwemo kununulia samani mbalimbali kiasi cha sh. 2,870,360, zimebainika kuyeyuka kifisadi kwa vile samani hizo hazipo.
 
Kwamujibu wa nyaraka zilizopeleka na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kipindi hicho wakati huo ikiwa Manispaa kwenda katika ofisi ya Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya,zinaonyesha kuwa fedha hizo zilitumika kununulia samani za ofisi ya mbunge wa Mbeya Mjini pamoja na kuikarabati kazi ambayo haikufanyika.
 
Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, Damson Ntangu akizungumza katika mahojiano na blogu hii ambayo ilitaka kufahamu fedha za kuhudumia ofisi za wabunge zinatumika vipi kwasababu ofisi ya mbunge wa Mbeya Mjini haina hata samani moja jambo ambalo hadi sasa limesababisha mbunge huyo kushindwa kukabidhiwa ofisi rasmi kuanza kazi ya kuwatumikia wananchi.
 
Alisema ingawa bado haijawekwa wazi jukumu la kuzihudumia ofisi za wabunge ni la nani, lakini hata hivyo Halmashauri ya Manispaa ya Mbeya kwa sasa Jiji, mwaka 2004/2005 ilitumia Sh.2,870,360 viti sita,Sofa kochi seti moja,meza kubwa moja,na zuria lenye ukubwa wa mita 15.
 
Ntangu alisema kutokana na hali hiyo madai yanayotolewa kwamba ofisi ya Mbunge wa Mbeya mjini haina samani wanaopaswa kulitolea maelezo ni Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambayo kwa mujibu wa nyaraka za barua ilieleza kuwa imetumia kiasi hicho cha fedha kununulia samani za ofisi hiyo.
 
Uchunguzi zaidi wa blogu hii umebaini kuwa  katika kipindi hicho pia kiasi cha  Sh,3,165,000 zilitolewa na serikali kuu ili zisaidie kuhudumia ofisi ya mbunge wa Mbeya mjini ambazo zilikabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na pia nyaraka hizo zinaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2006/2007 hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuhudumia ofisi ya mbunge.
 
Wakati utata ukigubika katika ofisi ya Mbunge wa Mbeya mjini, kwa upande wa ofisi ya Mbunge wa Mbeya vijijini (CCM),Mch.Luckison Mwanjale,ofisi yake ipo bomba ambapo kulingana na nyaraka zilizopo ni kwamba kwa mwaka 2004/2005  Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini,ilitumia Sh.10,300,000 kwa ajili ya kutengeneza na kununulia samani za ofisi hiyo kazi ambayo imefanyika kwa umakini mkubwa.
 
Kwaupande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya,Juma Rashid Idd, akizungumzia suala hilo alisema kimsingi ofisi za wabunge zipo chini ya Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya ambao ndio wanapaswa kutolea maelezo na kwamba Halmashauri inachokifanya ni kutoa ofisi hizo lakini huduma zote kwa maana ya kununua samani siyo jukumu la halmashauri.
 
Mbunge wa Mbeya Mjini,(Chadema), Joseph Mbilinyi,hadi sasa bado hajakabidhiwa ofisi kuanza kazi kwasababu ofisi iliyokuwa ikitumika na aliyekuwa mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Benson Mpesya, haina samani hata moja .
 
Ofisi hiyo ilibainika kwamba haina samani zinazotakiwa baada ya mbunge huyo kwenda kwa Mkurugenzi wa Jiji,Juma Rashid Idd kwa lengo la kukabidhiwa rasmi ili aanze kazi za kuwatumikia wananchi wa Jiji la Mbeya.
 
Ofisi hiyo ya mbunge ambayo ipo katika majengo ya zamani ya Halmashauri ya Jiji yaliyopo karibu na kituo Kikuu cha Polisi Mbeya mjini, mbali na kukosa samani muhimu, lakini pia hakukuwepo na makablasha (files) ambayo hutumika kuhifadhia nyaraka mbalimbali za kiofisi,ikiwemo mipango iliyotekelezwa na inayotarajia kutekelezwa na mbunge.

No comments:

Post a Comment