NA MZEE WA BONDE,TANGA
WANAFUNZI wanaosoma katika kituo cha Elimu cha Engusero cha Jijini Tanga wameutaka uongozi wa Kituo hicho kuwarudishia karo walizolipa kituoni hapo mwaka huu, ili wahamie katika vituo vingine kwa madai kuwa kituo hicho hakina walimu hali inayowafanya kila siku kufundishwa na mwalimu mpya.
Hali hiyo pia inadaiwa kumlazimu mkurugenzi wa kituo hicho PIUS YOHANA kuingia darasani katika baadhi ya siku ambayo anakuwa amekosa hata mwalimu mmoja na kufundisha yeye mwenyewe licha kuwa haiwezi kazi hiyo.
Hayo yalibainishwa wanafunzi hao jana baada ya kituo hicho kunyang’anywa madawati na vifaa vingine kama kompyuta na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo ndilo linalomiliki majengo ya kituo hicho tawi la Sabasaba, kufuatia deni la shilingi milioni 1.1 alilokuwa akidaiwa mkurugenzi huyo kama kodi ya Pango.
Kwa mujibu wa mmoja wa wanafunzi hao Mussa Kisoma, ada wanayotaka kurudishiwa na mkurugenzi huyo ni ile ya mwaka huu ambayo ni shilingi 280,000 kwa kila mwanafunzi, na kwamba kituo hicho kina takribani wanafunzi 400.
Ilidaiwa kuwa, baada ya kushindwa kulipa deni hilo kwa wakati, shirika la nyumba lilitoa tenda ya kutaifisha vifaa hivyo vya kujifunzia kwa kampuni ya udalali ya Jupiter, iliyofika kituoni hapo majira ya mchana na kuwatoa nje wanafunzi hao waliokuwa wanajisomea, kabla ya kuchukua madawati hayo na kompyuta na kuvipakiza katika lori.
Hata hivyo, wakati Jupiter wakitekeleza zoezi hilo , mkurugenzi huyo alifanikiwa kulipa deni hilo mara moja kwa mmliki huyo na kuruhusiwa kuendelea kutumia jengo hilo .
Meneja wa shirika la nyumba la Taifa Mkoani Tanga, Damas Ngoiya alithibitisha mpangaji huyo kulipa deni hilo na kuruhusiwa kurudisha vifaa vyake katika jengo hilo , ikiwa pia ni baada ya kuilipa kampuni ya udalali iliyofanya kazi ya kukusanya vifaa hivyo.
“Naomba wateja wajenge tabia ya kulipa mapema kodi zao…hakuna haja ya kufikia hatua ya kunyang’anyana kwa kuwa ni usumbufu hata kwetu sisi” alisema Ngoiya.
Akizungumzia madai ya wanafunzi hao kutaka warudishiwe karo zao ili wakasome katika vituo vingine, mkurugenzi huyo alisema kuwa, hawezi kulitolea majibu ya haraka suala hilo kwa kuwa wanafunzi hao wamekwishatimiza sehemu kubwa ya mwaka wa masomo ikiwa ni pamoja na kusoma silabasi zote kwa baadhi ya masomo.
“Kwa sasa niko katika vikao na wenzangu siwezi sina majibu ya ya moja kwa moja lakini kimsingi mwaka wa masomo karibu unaisha na baadhi ya masomo wamemaliza silabasi” alisema mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, wanafunzi hao waliandama hadi katika ofisi za elimu za jiji la Tanga kuwasilisha kilio chao hicho na kuahidiwa kuwa, uongozi wa jiji utalifanyia kazi suala hilo .
No comments:
Post a Comment