Na Mzee wa Bonde
TAASISI ya kiraia inayojishughulisha na masuala ya kijamii katika wilaya ya Pangani mkoani Tanga ya Uzikwasa imeanza kutekeleza mpango wa ukarabati wa majengo ya kale wilayani humo kwa lengo la kuyahifadhi ili yaendelee kuwa sehemu ya vivutio vya utalii na kumbukumbu ya wilaya hiyo kongwe.
Afisa ufuatiliaji na Tathimini wa taasisi hiyo Joseph Mushi alisema kuwa, wameamua kuchukua jukumu kama sehemu ya shughuli za kijamii na kwamba ukarabati huo utasaidia kuyafanya majengo hayo yaendelee kuwavutia watalii na kuhifadhi historia ya wilaya ya Pangani.
Alisema mpango huo ni mojawapo ya programu mbalimali za kijamii wanazozitekeleza kwa wakazi wa wilaya hiyo, ikiwemo ile ya kupambana na mimba za wanafunzi, pamoja na ndoa za umri mdogo.
Akielezea kampeni hiyo, mratibu wa Programu za kijamii wa taasisi hiyo Nickson Lutenda alisema kuwa, wakazi wa wilaya hiyo wameonesha mwamko mkubwa katika kampeni hiyo iliyolenga katika mabadiliko ya tabia kupitia njia za kuonesha filamu na videkezo vya video.
“Wananchi wanafurahishwa sana katika vijiji vyote ambako tunaendesha programu hizo na tumeibua kesi nyingi sana za wanafunzi kukatisha masomo kwa kupewa mimba…katika kijiji cha Mzambarauni baadhi ya wanafunzi waliokatisha masomo kwa kupewa mimba walitoa ushahidi wa wazi wa tatizo hilo” alisema.
Alisema kuwa, kwa ujumla taasisi hiyo imedhamiria kupambana na matatizo yanayowakabili watoto na wanafunzi wa kike wilayani humo, ikiwemo ndoa za kulazimishwa hasa kwa wasichana na wanafunzi wa kike, mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo, pamoja na ubakaji wa vikundi hali inayopelekea maambukizi ya ukimwi na kukwamisha vijana wengi kuendelea na masomo.
No comments:
Post a Comment