MAJONGOO BAHARI YAKIWA KWENYE OFISI ZA MACEMP ZILIZOPO JIJI LA TANGA. |
IDARA ya Uvuvi kwa kushirikiana na Mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Mwambao wa Pwani (MACEMP) Wilayani Mkinga, inawasaka wavuvi wanaodaiwa kuwa Wazanzibar wanaoendesha uvuvi haramu wa kutumia baruti na kuvua majongoo bahari yaliyozuiwa na serikali.
Wazanzibar hao wanaodaiwa wamefika katika vijiji mbalimbali vya ukanda wa bahari ya hindi ya wilayani hapa wakiwa na vibali vya kuvua samaki aina ya pweza, wanasakwa baada ya kubainika kuvua majongoo bahari yapatayo 82 yenye wastani wa uzito wa kilogram 132 na thamani ya shilingi mlioni 3.3.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mratibu wa Mradi wa MACEMP Bw. Sylevester Givver alisema kuwa Wazanzibar hao walifika katika kijiji cha Mongavyeru kilichopo mpakani mwa Kenya na Tanzania kwa ajili ya uvuvi ujulikanao kwa jina la Dago, wamekuwa wakijihusisha na uvuvi haramu ukiwemo kuvua majongoo hayo bahari.
Alisema walifuatilia kwa kufanya doria usiku kuwasaka wavuvi haramu hao na ndipo walipofika kwenye nyumba moja huko Mongavyeru inayomilikiwa na mama aliyemtaja kwa jina la Tima Mohamed ambaye walipofika kundi la wanaume wavuvi walitoroka na hivyo kumtia mbaroni mwanamke huyo.
"Tulipompekua humo ndani tulikuta majongoo bahari yapatayo 82 yaliyokuwa na uzito kama kilogramu 132 hivi unajua majongoo haya kilo moja huuzwa kati ya sh. 20,000 hadi 25,000...Pia mle ndani tulikuta chupa 19 za gesi na chupa nne za baruti, ile nyumba ilikuwa imefungwa milango yote," alisema Bw. Givver ambaye wavuvi wilayani humo wamekuwa wakimsifu kwa jitihada zake za kuwapa mafunzo na mbinu mbalimbali za uvuvi wa kisasa.
Majongoo bahari kwa mujibu wa Givver, hivi sasa kuna mkakati wa kidunia uliopitishwa kuwalinda viumbe hao waliokuwa katika hatari ya kutoweka, wamekuwa wakiuzwa kwa wingi katika nchi za China, Hong Kong, Philipine na Vietnam ambako licha ya matuminzi ya chakula, utengenezaji peremende, soli za viatu na matumizi mengine, pia hutumika kutolea mahali kwa wanaume wanapotaka kuoa.
Hata hivyo, Ofisa huyo alisema mbali na kuwasaka wavuvi hao pia wamebaini kwamba wavuvi wanaotumia baruti na zana zilizokatazwa na serikali, wamekuwa wakitoka wilayani Tanga eneo la Kasera na Ngome Kisosora wanaotumia mwanya kuvua kwa kutumia baruti hatua ambayo tayari wanafanya doria ya mara kwa mara ili kudhibiti uvuvi huo.
No comments:
Post a Comment