Na Mashaka Mhando,Tanga
WAGOMBEA wa ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majimbo ya Handeni, Mlalo na Mkinga, wameshinda kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya kuwabwaga wapinzani wao wa vyama vya CUF na Chadema waliokuwa na wagombea.
Wakitangaza kwa nyakati tofauti Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la handeni Bw. Hassain Mwachibuzi, alisema Dkt Abdallah Kigoda mbunge mkongwe wa CCM ameshinda baada ya kupata kura 31,497 dhidi ya mpinzani wake wa chama cha chadema Saleh Mbwetto aliyepata kura 5,907 na mgombea wa CUF Aidano Shundi aliambulia kura 4,947.
Jimbo la Mlalo msimamizi wa uchaguzi Bi Lucy Msofe alimtangaza mgombea wa CCM Brigedia jenerali (Mstaafu) Hassain Ngwilizi ambaye alipata kura 24,122 dhidi ya kura 5,337 za mpinzani wake wa karibu mwandishi wa habari wa siku nyingi Bw. Charles Kagonji wa chama cha chadema ambaye alijiunga na chama hicho baada ya kushindwa kwenye kura za maoni na Ngwilizi. Bw. Gogola Sechonge wa CUF aliambalia kura 1,695.
Jimbo la Mkinga, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Bw. Filbert Ngaponda, alisema bw. Dastan Luka Kitandula wa CCM ameshinda kwa kura 19,667 dhidi ya mpinzani wake wa CUF Bw. Bakari Mbega aliyeambulia kura 11,252 kati ya kura halali 30,919 kati ya watu 31,647 waliojitokeza kupiga kura kati ya watu 64,833 waliojiandikisha kupiga kura katika jimbo hilo.
Akitangaza kura za rais Bw. Ngaponda alisema mgombea wa CCM Jakaya Kikwete alipata kura 22,803 sawa na asilimia 73.62, mgombea wa CUF Profesa Ibrahimu Lipumba alipata kura 6,484 mgombea wa chadema Dkt Willbroad Slaa kura 1,083 na mgombea wa PPT-Maendeleo Bw. Kuga mziray alipata kura 485.
Wagombea wengine ni wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 54, mgombea wa UPDP Bw. Dovutwa fahm kura 35 na mgombea wa TLP Bw. Mutamwega Mugaya aliambulia kura 33.
No comments:
Post a Comment