Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach

Blogu hii imedhaminiwa na Simba Video Coach
Kwa usafiri wa Dar es salaam, Morogoro, Dodoma na Arusha, safiri kwa raha na Simba Mtoto Luxury Coach

Monday, November 29, 2010

TAMISEMI YAIAGIZA HALMASHAURI KYELA KUMLIPA ALIYEKUWA MWENYEKITI WAKE

Na Mdau Thobias Mwanakatwe, Kyela
WIZARA ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeiweka katika wakati mgumu Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya baada kuiagiza kumlipa stahili zake zote aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Timoth Kisugujila  kutokana na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kumvua madaraka mwenyekiti huyo bila kuzingatia taratibu na sheria za TAMISEMI.
 
Kisugujila ambaye alikuwa diwani wa kata ya Makwale wilayani hapa, alivuliwa madaraka ya uenyekiti Novemba mwaka jana na kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa kudaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kumwandikia barua aliyekuwa diwani wa kata ya Kyela mjini,Visk Mahenge kwamba udiwani wake umekoma kutokana na kata ya Kyeka kupandishwa hadhi kuwa Mamlaka ya Mji mdogo.
 
Katika barua yake aliyekuwa Mwenyekiti huyo wa halmashauri, yenye kumb Na KDC/1/09 ya Novemba 13 mwaka 2009  ilieleza  kuwa kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 kifungu cha 45 (1) inayoongoza uundwaji wa Mamlaka ya Miji Midogo inapelekea kumnyima fursa ya yeye diwani (Visk Mahenge) kuendelea na madaraka yake ya udiwani.
 
Kutokana na barua hiyo ya Kisugujila, madiwani waliokuwa na hoja ya kumuengua mwenyekiti walimuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Mhando Senyagwa aiitishe mkutano wa dharura ndani ya siku nne ambapo Mkurugenzi alifanya hivyo na madiwani hao kwa kauli moja wakamwazimia na kumuengua katika nafasi ya uenyekiti.
 
Baada ya azimio hilo la madiwani kufikiwa,Mkurugenzi wa Halmashauri,Senyagwa aliitisha kikao kingine cha Baraza la Madiwani na kumchagua Mwenyekiti mpya wa Halmashauri, Watson Majuni ambaye alikuwa Makamo Mwenyekiti na Diwani wa kata ya Kajunjumele ambaye aliidhinishwa rasmi kuwa Mwenyekiti.
 
Kikao hicho cha kumuidhinisha Mwenyekiti mpya wa Halmashauri hiyo,kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, ambaye katika hotuba yake alisema amefurahishwa na uamuzi uliofikiwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa kumwadabisha Mwenyekiti wao,Kisugujila kwa kosa la kutumia madaraka yake vibaya.
 
Kwamujibu wa barua yenye kumbu Na.CHB.215/443/01/61 ya Novemba 5 mwaka huu iliyoandikwa na Waziri wa TAMISEMI, Celina Kombani kwenda kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela na nakala kupelekwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,imetoa maamuzi ya rufaa iliyokatwa na Kisugujila ya kupinga kuvuliwa uenyekiti wa halmashauri.
 
Katika maamuzi ya waziri yaliyozingatia sababu moja kati ya nne zilizotolewa na mlalamikaji (Kisugujila), kuwa taarifa ya Mkutano wa Baraza  la Madiwani lililomvua madaraka  haikuzingatia masharti ya Kanuni ya 3(c)  ya mwaka 1995 ya taratibu za kumuondoa madarakani  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya.
 
“Kuhusu sababu ya nne ya rufaa imedhihirika kuwa hakuna taarifa ya maandishi iliyopelekwa kwa Mkuu wa Mkoa na kwamba Mkuu wa Mkoa au mwakilishi wake hawakuhudhuria mkutano huo,kutokuwepo kwa Mkuu wa Mkoa au mwakilishi wake katika mkutano huo ni kukiuka masharti ya kanuni ya 3 (c) ya taratibu za kumuondoa madarakani Mwenyekiti wa Halmashauri,”imeeleza barua hiyo ya Waziri wa TAMISEMI ambayo NIPASHE inayo nakala yake.
 
Barua hiyo imeeleza kwa msingi huo uamuzi uliofanywa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela bila kuwepo Mkuu wa Mkoa au mwakilishi wake ni batili na hivyo waziri mwenye dhamana na serikali za mitaa ameamua kuwa rufaa ya Kisugujila ya kupinga kuvuliwa Uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo imekubaliwa.
 
Kwamujibu wa barua hiyo ya waziri wa TAMISEMI,imeendelea kueleza kuwa kwa kuwa muda wa vikao vya mabaraza umeishia mwezi Julai 2010, hivyo Kisugujila atahesabika kuwa alikuwa madarakani kuanzia tarehe alipovuliwa uenyekiti wa halmashauri hadi tarehe ya mabaraza yalipovunjwa.
 
Kutokana na uamuzi huo,Waziri wa TAMISEMI amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela,Mhando Senyagwa kumlipa stahili zake zote za uenyekiti Timoth Kisugujila,  kuanzia tarehe alipovuliwa madaraka hadi mwezi Julai 2010 mabaraza yalipovunjwa.
 
Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI aliyefahamika kwa jina moja la Maswi, alipozungumza na NIPASHE kwa simu alisema pamoja na kwamba suala hilo lipo lakini hawezi kulizungumzia na badala yake Katibu Mkuu wa TAMISEMI ndiye anapaswa kulitolea maelezo ya kina.
 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela,Senyagwa alipofuatwa na NIPASHE ofisini kwake kuzungumzia sakata hilo ilishindikana kutokana na kupata shinikizo la damu ghafla ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya Kyela baada ya kupata ghafla ugonjwa wa shinikizo la damu.
 
Kwamujibu wa taarifa zilizopatikana toka hospitalini hapo ambazo zilielezwa na wauguzi wa hospitali hiyo ambao waliomba majina yao yasiandikwe gazetini walisema hali ya Mkurugenzi si nzuri na kwamba shinikizo la damu lilikuwa limepanda hadi kufikia 220 kwa 160.
 
Kuugua ghafla kwa Mkurugenzi huyo kumezua maswali mengi kutoka kwa wafanyakazi wa halmashauri hiyo hasa ikizingatia kuwa imekuja siku tatu tu baada ya kupokea barua hiyo toka wizarani.
 

No comments:

Post a Comment