TAARIFA RASMI KWA VYOMBO VYA HABARI NOVEMBA 5, 2010
Novemba 3,2010 mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt Willbroad Slaa aliwatuhumu makada 30 wa Chama Cha Mpinduzi (CCM) kuwa walifanya kikao cha kupanga kumwibia kura mjini Mwanza. Kati ya makada aliowatuhumu ni pamoja na mimi.
Napenda kuufahamisha umma kuwa habari hizi siyo za kweli kwasababu mwezi wote wa Oktoba nilikuwa jimboni kwangu nikifanya kampeni za kuwania ubunge jimbo la Mondoli. Sikupata kusafiri kwenda Mwanza hata siku moja, na siku iliyotajwa ya Oktoba 19, nilikuwa kwenye vijiji vya Mfereji na Enguiki nikifanya kampeni siku nzima.
Ukiacha tuhuma hizo, pia upo uvumi uliosambazwa kwambanilishiriki kikao cha mkakati wa kuchakachua kura, mjini Arusha kumsaidia mgombea wa chama cha mapinduzi (CCM) Dkt Batilda Burian, aweze kushinda kiti hicho. Nasema uvumi huo ni uzushi na siyo wa kweli.
Kutokana na yote haya, ninakwazika kwamba inaonekana katika nchi yetuumeanza kuingia utamaduni mpya wa kufanya siasa za uongo, uvumi, uzushi na kila aina ya hila kwa nia ya kujipatia ushindi. Kwa udhoefu wa mataifa mengine yaliyotuzunguka, ndani ya Afrika na sehemu nyinine duniani, amani hupotea kutokana na usambaji wa taairifa za uongo.
Mwasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alituachia amani na utulivu ambavyo ni tunu ya Taifa hili. Dalili zinazoonekana, kuna watu wanaelekea kuchoshwa na amani iliopo. Wanajianda kufanya vurugu, kuliiingiza taifa hili katika machafuko, na sijui wanafanya hivyo kwa maslahi ya nani.
Wito kwa Watanzania, ni kwamba tusiichoke amani. Amani tuliyonayo ndiyo iliyotutofautisha na mataifa mengi yaliyotuzunguka na kuifanya Tanzania nchi ya kupigiwa mfano. Tuelekeze nguvu zetu katika shughuli halali za kutuletea kipato zisizoharibu amani yetu. Tukiiharibu amani tuliyonayo, mwisho wa siku nchi yetu itatekeketea na sote hatutakuwa salama. Tutakuwa tumekwisha.
Mwisho, Namsihi Dk Slaa ajipe muda wa kuzifahamu vyema siasa za nchi hii. Asidanganywe na mahudhurio ya mikutano ya hadhara akadhani ndizo kura katika masanduku ya kupigia kura. Namsihi ajifunze zaidi jinsi ya kufanya siasa za kistaarabu bila kueneza, uvumi, uongo, chuki na uzushi vyenye kutetelesha amani ya nchi yetu. Mungu ibariki Tanzania.
EDWARD LOWASA, Mbunge Mteule jimbo la Mondoli.
No comments:
Post a Comment