Mh Sambwee Shitambala
MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya,Sambwee Shitambala ambaye pia alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Mbeya Vijijini amejiuzuru nafasi hiyo kutokana na kutuhumiwa kuwa amehogwa Sh.Milioni 600 na Chama cha Mapinduzi (CCM) na hivyo kusababisha ashindwe kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo hilo.
Ametangaza uamuzi huo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea tathimini ya uchaguzi mkuu wa uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu mbela ya Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya,Eddo Makata na Kaimu Mwenyekiti wa Vijana Chadema mkoa,Exavery Mwalembe.
Shitambala alisema amechukua uamuzi wa kujiuzuru nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Chadema mkoa ili kupisha uchunguzi uweze kufanyika ndani ya chama kufuatia tuhuma zambazo zinaelekezwa kwake kwamba kushindwa kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini kumetokana na kuhongwa fedha na CCM.
Alisema shutuma zinazoelekezwa kwake ambazo pia zinatolewa na wanachama wa Chadema na viongozi zimemshushia hadhi mbele ya jamii na utendaji wake wa kazi ya uwakili kama mwanasheria hivyo njia pekee aliyoamua kuchukua ni kujiuzuru nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya kwa lengo la kupisha uchunguzi uweze kufanyika kubaini kama kuna ukweli wa tuhuma hizo.
“Maneno yanayozungumzwa kwamba nimehongwa fedha yamepunguza imani kubwa sana kwa wananchi ambapo sasa wamesahau hata mambo mazuri niliyofanya ya kukijenga chama mkoa wa Mbeya,kutokana na hali hiyo nimeona ni bora niachie ngazi na nitabaki kuwa mwanachama wa kawaida ndani ya chama,”alisema Shitambala.
Alisema tangu kumezuka uvumi huo ndani ya chama,amejaribu kumpigia simu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema,Freeman Mbowe, lakini bahati mbaya hapokei simu jambo ambalo linanisikitisha na kutoamini kama ni kweli muda wote anakuwa bize kiasi kwamba ashindwe kupokea simu yangu.
Alisema kinachompa mashaka ni kwanini tuhuma za kuhongwa fedha na CCM zinaelekezwa katika jimbo la Mbeya vijijini wakati yapo majimbo kama Songea, Njombe, Segerea, kilombero, Arumeru, Kiteto, Busanda, Bukoba na Tarime ambayo Chadema ilikuwa na uhakika wa kuibuka na ushindi lakini wagombea wake wameshindwa na hakuna tuhuma kama hizo.
Shitambala alisema kutokana na kuwepo kwa tuhuma hizo zinazoelekezwa kwake tu anaamini kuwa kuna jambo limejificha ndani yake hasa ikizingatia kuwa hii ni mara ya pili kutuhumiwa hivyo ambapo mara ya kwanza ilikuwa wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini uliofanyika mwezi Januria 2008.
Katika uchaguzi huo mdogo Shitamba aliondolewa kugombea ubunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kukosea mashariti ya kiapo ambapo badala ya kuapa mahakamani aliapa kwa wakili kitu ambacho kinapingana na kanuni za viapo vya uchaguzi na hivyo kukaibuka maneno kwamba alihongwa fedha na CCM ili afanye makosa hayo hasa ikizingatia kuwa ni mwanasheria anayefahamu sheria.
Shitambala alisema kimsingi yapo mambo mengi yaliyosababisha ashindwe kwenye kinyang’anyiro cha ubunge uchaguzi wa mwaka huu ikiwemo jiografia ya jimbo la Mbeya vijijini na pia baadhi ya mawakala wake hususani wa kata ya Inyala ambao walikimbia na hawajulikani waliko hadi sasa.
“Mambo yaliyochangia nijitoe ni kutuhumiwa kwa mara ya pili hivyo nadhani watu wa Mkoa wa Mbeya ni wapenda majungu hivyo hakuna haja ya kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa ,tuhuma ya kwamba sikuweka mawakala siyo za kweli niweka mawakala kila kituo na nikawalipa japo wapo waliokimbia na mpaka leo hii tunaendelea kuwatafuta,”alisema Shitambala.
Alisema wakati umefika kwa wanachama wa Chadema wawe wanajenga imani kwa viomngozi wao kwa kutambue kuwa nguvu ya mgombea wao ikoje kwa mpinzani wake badala ya kuwa wepesi wa kupokea propaganda na wepesi wa kumeza ndoani.
Aliongeza kuwa kwa hali iliyojitokeza Mbeya inawezekana propaganda hii ya kwamba amehongwa fedha ili kuuza jimbo ilienezwa na mtu mmoja tu lakini wanachama wengi wamechukulia kama ni jambo la kweli hali ambayo ni hatari kubwa kwa chama.
Shitambala alisema wana Chadema wafahamu kuwa kamwe hawezi kuuza heshima yake kwa pesa maana yeye si Malaya wa siasa kwani anategemea busara zangu si kwa pesa.
Alisema pamoja na kujiuzuru kwake hana mpango wa kuhamia chama chochote cha siasa na kwamba kama ataamua kuhamia chama kingine cha siasa itakuwa ni maamuzi yake hayatakuwa maamuzi ya kununuliwa.
“Sina wasiwasi na maisha kiasi kwamba mpaka nikubali kununuliwa kirahisi.iwe CCM, TLP au chama chochote cha siasa wakinitaka sitawakubalia nitabaki kuwa mwanachama wa Chadema japo vyama vingi vimekuwa vikinitaka lakini sina mpango wa kwenda chama chochote ikitokea ni maamuzi yangu,”alisema Shitambala.
Hata hivyo kujiuzuru kwa Shitambala kumeelezwa na wachambuzi wa masuala ya kiasia kwamba itakuwa ni pigo jingine kwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Mr. Sugu ambaye kimsingi kuchaguliwa kwake kumetokana na msaada wake mkubwa.
Pia uamuzi huo wa Mwenyekiti wa Chadema mkoa ni pigo na athali kwa chama hicho mkoa wa Mbeya kwani katika kipindi cha mwaka huu viongozi wawili wamejiuzuru na kufukuzwa ambapo wa kwanza alikuwa ni Ipyana Seme ambaye aliyekuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Mbeya Vijijini ambaye alifukuzwa na viongozi wa makao makuu ya chama .
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu uliomalizika Oktoba 31 mwaka mgombea wa CCM, Mchungaji Luckison Mwanjale aliibuka kidedea wakati nafasi ya pili ilishikiliwa na Sambwee Shitambala wa Chadema.
No comments:
Post a Comment