Na Mashaka Mhando,Korogwe
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Korogwe Mji kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw. Yusuph Nasir almaarufu 'Obama', ametangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho katika uchaguzi uliofanyika jana baada ya kuwashinda wagombea wengine watatu wa vyama vya upinzani.
Akitangaza matokeo hayo leo saa 5:00 asubuhi Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo Bi Christina Midelo alisema Obama amepata kura 12,090 kati ya kura 15,346 ya wapiga kura wote waliojiandikisha na kura 62 ziliharibika.
Bi Midelo alisema kuwa mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Kalistus Shekibaha alipata kura 1,720, mgombea wa Chama Cha Wananchi (CUF) Bw. Juma Mgogo alipata kura 400 na mgombea wa chama cha SAU Bw. Tony Kamuhanda aliambulia kura 225.
Akitangaza matokeo ya urais, Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema mgombea wa CCM Bw. Jakaya Kikwete aliongoza kwa kupata kura 10,761, Dkt Wilbrod Slaa wa Chadema alipata kura 3,435, Profesa Ibrahim Lipumba alipata kura 394, Bw. Kuga Mziray wa APPT-Maendeleo kura 110, NCCR-Mageuzi mgombea wake Bw. Hashim Rugwe alipata kura 19, mgombea wa TLP Bw. Mutamwega Mugaya alipata kura 5 na mgombea wa UPDP Bw. Dovutwa Fahm alipata kura 4.
Obama ambaye alimshinda Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw. Joel Bendera mara baada ya kutangazwa mitaa mbalimbali ya mji wa korogwe vijana mbalimbali waling'ara kwa kupanda pikipiki mitaani, mgombea huyo alisema atahakikisha changamoto zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo, atazifanyia kazi ikiwemo kutekeleza ahadi alizozitoa kama zilivyoaanishwa kwenye ilani ya CCM.
No comments:
Post a Comment