Wananchi Korogwe watakiwa kubadili tabia-DC
*kuwa na nyumba ndogo siyo dili
*Ukiweza kuandaa mwanamke na kondomu pia ukumbuke
Na Mashaka Mhando,Korogwe
MKUU wa wilaya ya Korogwe Bw. Erasto Sima, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kubadili tabia kwa kupunguza 'nyumba ndogo' ili kuepuka maambukizo ya ugonjwa hatari wa UKIMWI na wajitahidi kuzuia maambukizi mapya kama ambavyo mkoa wa Kagera ulivyoweza kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo hapa nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji juu ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI mahali pa kazi kwa watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alisema suala la kuwa na nyumba ndogo limepitwa na wakati hivyo ni vema watumishi na wananchi wa wilaya hiyo kwa ujumla wao, wakabadili tabia kwani ugonjwa huo umekuwa ukipoteza nguvu kazi ya Taifa kutokana na kukosekana kwa tiba yake hadi sasa.
Alisema kwenye miaka ya 1993 hadi 1994 mkoa wa Kagera ulikuwa ukishika namba moja nchini kwa kuwa na wagonjwa wengi lakini hivi leo mkoa huo umeshuka hadi kufikia wa nne kitaifa hatua ambayo inatakiwa kuchukuliwa na wananchi wa wilaya hiyo kwa vile suala la ugonjwa huo ni mtu mwenyewe kubadili tabia ya wapenzi alionao.
"Kagera ilikuwa ya kwanza nchini kwa kuwa na wagonjwa wengi wa UKIMWI hapa nchini, leo hii imeshuka tuige baada ya wananchi wake kufuata elimu waliyopewa...Ni vema na sisi Korogwe tukaiga mfano huo huu mpango wa mtu kuwa na nyumba ndogo nyingi hauna maana yoyote kwanza hizi ni nyumba kubwa maana zinatutesa kuliko wake zetu," alisema Bw. Sima na kuwataka watumishi hao endapo hawataki kuwaacha tendo hilo wafanye maandalizi ya kutumia kondomu badala ya kufanya ngono zembe.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Bw. Lameck Masembejo alisema watumishi zaidi ya 2,000 wa wilaya hiyo tayari wamepatiwa semina kuhusu ugonjwa huo na kwamba aliwahamasisha kupima na kutambua afya zao na kutoa taarifa endapo miongoni mwa kutabainika wagonjwa ili halmashauri iweze kutoa msaada ikiwemo ruhusa ya kwenda kuchukua dawa na matuminzi yake.
Naye mratibu wa mafunzo ya UKIMWI pahali pa kazi Bw. Federick Linga alisema lengo la kuwapatia elimu ya kuhusu ugonjwa huo kupitia mradi wa maboresho na tawala bora (SULGO), watumishi ni kutaka wajitambue nakupima ili waweze kupata huduma za magonjwa hayo na kisha kuhamasisha upimaji wa hiari ambao utasaidia watumishi kujali afya zao baada ya kupima maambukizi hayo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment