Injinia Omar Nundu 'Zindaa moja ya picha yake iliyokuwa imetawala kwenye mitaa mbalimbali ya Jiji la Tanga. |
Wafurahia Omar Nundu kupata Uwaziri na Ummy
Na Mashaka Mhando
BAADHI ya wananchi wa Jiji la Tanga wamempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuunda baraza ambalo wana amini litaleta tija na maendeleo ya Watanzania kwa kuwepo sura mpya ambazo zimewapa matumaini ya kufanya vizuri katika miaka mitano ya serikali ya awamu ya Nne.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wananchi hao wamesema Baraza hilo ni dogo na lenye sura mpya za viongozi ambao kimsingi wengi wao wanakubalika kiutendaji na hivyo kuwapa matumaini makubwa watanzania kwa kutegemea mabadiliko chanya hapa nchini.
“Kweli Rais tunampongeza na hawa aliyowachagua wanatakiwa kujenga uaminifu wa Rais na wafanye kazi kwa nguvu zao zote ili maendeleo yaweze kupatikana aktika taifa hili…Baraza hili ni dogo hivyo ni rahisi kwa Rais na Waziri Mkuu kulimudu lakini kubwa zaidi ni sura mpya ambazo zimeonekana wataweza kubadili sura iliopo ya kiutendaji zaidi “,alisema Mzamin Shemdoe.
Hata hivyo wananchi hao wametoa angalizo kwa Viongozi walioteuliwa kuunda Baraza hilo kwamba hawategemei kutokea kwa misukosuko kama ilivyotokea katika kipindi ya kwanza cha uongozi wa awamu hii ya nne iliyopelekea kuvunjwa kwa baraza hilo la mawaziri kutokana baadhi yao kukabiliwa na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu wa fedha za umma.
Bw. Said Abdalah alisema kilichotokea katika baraza la kwanza la awamu ya Nne ilikuwa ni pigo kwa Taifa na kwa kiasi fulani misukosuko ile ilichangia kurudisha nyuma maendeleo ya watanzania hivyo ni vema Mawaziri walioteuliwa wabadilike kwa vile Watanzania sasa wamekuwa weledi wa masuala ya kisiasa na wafatiliaji wa kazi zao.
Walisema wanatarajia viongozi walioteuliwa kuwa watu waadilifu na wawajibikaji zaidi ili kulinda uminifu waliowekewa na Rais na watanzania kwa ujumla ili hatimaye waweze kutekeleza ahadi zilizowekwa wakati wa uchaguzi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho pamoja na kunadi ilani yake hiyo pia Rais alikuwa na ahadi za papo kwa pao hivyo viongozi hao wanatakiwa kuzifuatiliwa kwa karibu utekelezaji wake.
Mwanaharakati wa masuala ya maendeleo Bw. Josephat Torner alisema kuwa kundi la walemavu lilitegema masuala yao yangeweza kuhamishwa kutoka katika Wizara ya afya na ustawi wa jamii na kupelekwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu kutokana na imani waliyonayo watu wenye ulemevu kwa Waziri mkuu kwa kuwa mstari wa mbele katika kutatua matatizo na kero zinazowakabili.
Bw. Torner alisema hatua hiyo ingewezesha masuala ya watu wenye ulemevu kuwa mtambuka zaidi kwani yangekuwa yakipewa kipaumbele tofauti na yanavyoshughulikiwa katika Wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa sasa.
Katika hatua nyingine wananchi hao wamepongeza Rais kwa kuwachagua wabunge wawili wa mkoa huo kuingia katika baraza hilo la mawaziri ambapo mbunge wa Tanga mjini Bw. Omari Nundu 'Zindabaa' ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi na Mbunge wa Viti maalum Bi Ummy Mwalimu amekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya maendeleo ya jamii Jinsia na watoto.
"Rais amefanya vizuri sana na tunampongeza kwa kumpa Mbunge wetu Bw. Nundu (Omar) wizara ambayo iotashughulikia pia Bandari hivyo tunaamini kwamba bandari ya Tanga ambayo imewekwa kwenye ilani ya uchaguzi kujengwa kwa kina kirefu, mbunge wetu atasimamia na ujenzi wake utafanyika," alisema Bi Hadija Mohamed mkazi wa Chumbageni.
Nundu zindaba safiiiiiiiiiiiiiii
ReplyDelete